MAHAFALI YA NANE;CHUO CHA UALIMU NAROK.
Wanafunzi pamoja na waliohudhuria sherehe hii ya mahafali wakisubiri ianze katika Chuo cha Ualimu cha Narok

Wanafunzi 614 wamehitimu leo hii kutoka Chuo cha Ualimu ndani ya kaunti ya Narok ikiashiria kukamilisha masomo rasmi na kujiandaa kwa ajili ya kulitumikia taifa hili. Kwa miaka mwili au mitatu kulingana na kitengo cha kila mmoja,wanafunzi hawa walipata kuingia mwituni na leo hii ni wazi kwamba baadhi yao wamepata kurejea na kuni ambazo kwa hakika zitawafaidi pakubwa katika siku zao za usoni.


Wanafunzi hao wakiwa katika kanzu za mahafali walionyesha furaha na kuridhika kwa siku hii walioisubiria bila ya kujuta tangu mwaka jana walipomaliza kuudhuria masomo yao. Wanatumaini kupata kazi kwa sababu wameshakabidhiwa vyeti vyao vya kuhitimu tofauti na vyuo vingine ambapo wanafunzi huchukua vyeti vyao baadaye mbali na siku yao ya kuhitimu. Cynthia Chemtai mmoja wa waliohitimu anasema, "sina shaka nitapata kazi maanake sifa zote na ujuzi unaotakikana ninao," hii ni hakikisho kwamba wanafunzi hawa wapo tayari kuwajibikia nchi yao iwapasavyo.
Wanafunzi waliokuwa wanahitimu katika Chuo cha Ualimu Narok wakiwa wameketi tayari kupata maagizo na vyeti vyao kutoka kwa mgeni mkuu Dkt. Richard Belio Kipsang'.  Picha/lydia


Mwalimu mkuu Bi. Irene Nyaga ambaye pia ni katibu wa bodi ya usimamizi ya Chuo hiki,aliwapongeza waliokuwa wanahitimu na kusema kwamba inajumuisha bidii ya serikali, wasimamizi mbali mbali wa elimu,bodi ya usimamizi,walimu na wanafunzi wa Chuo hiki kufika mahali walipo. Aliwashauri na kuwakumbusha kwamba hii ni hatua ya kwanza katika safari yao ya mafanikio makubwa. "Kila mnapopata nafasi,tieni bidii iwe ni katika elimu au vitengo vingine na mkaipende  kazi yenu,"alisema. Mbali na ushauri huu, Bi. Irene Nyaga alisisitiza kuwa wahitimu wote wanafaa kutilia maanani mienendo ya sasa katika elimu kama vile 'Competence Based Curriculum ', hoja ambayo ilisisitizwa zaidi na naibu wa mwalimu mkuu wa Chuo hiki Bwana Chebogut J.K.


Mkuu wa kitivo cha mtaala alimkaribisha mgeni mkuu Daktari Richard Belio Kipsang' ambaye ni katibu mkuu katika Idara ya Taifa ya Mafunzo ya Mapema na Elimu ya Kimsingi, Wizara ya Elimu. Dkt. Belio Kipsang' aliwapongeza wanafunzi kwa kukamilisha masomo yao ya ualimu na kisha kuwaagiza kuitumikia nchi kwa kujitolea.


Ingawa ilikuwa furaha kuhitimu, kwa upande mwengine ni huzuni kwa kuwa kuna baadhi ya wanafunzi zaidi ya mia mbili ambao hawakuweza kuhitimu na wenzao kwa sababu ya kufeli katika mitihani yao na wengine kwa kukosa kukamilisha karo ya shule. Waliofeli hili lilikuwa pigo la kuwaamsha ili wapate kusugua vyao pia vipate kung'aa kama vile wenzao maanake kizuri kinaundwa na kuvunjika kwa mwiko hakumaanishi ni mwisho wa kusonga ugali.


Hata baada ya wanafunzi 614 kuhitimu swali labaki kuwa je,serikali ipo tayari kuwapokea walimu hawa na kuwapa kazi kulingana na matumaini ambayo wameishi kwayo?

Comments

Post a Comment

Leave a comment

Popular posts from this blog

MOTHERLAND