BWAWA LA KESSES, TEGEMEO LA WENGI.
Kwa miaka michache iliyopita kituo cha Kesses kimezidi kuwa kwa idadi ya watu,kutangamana kati yao kibiashara na hata kiteknolojia. Hii imepelekea uchumi kunawiri na hivyo basi kuboresha maisha ya wakaaji wa Kesses na hata majirani. Licha ya kuwa na haya maendeleo yote,ni jambo la kuvutia kwamba bwawa la Kesses ambalo lipo umbali wa kilomita saba kutoka kwa kituo hiki ndilo chanzo cha ukuaji wa vitu vyote hivi. Ni wazi kwamba yapo mengi ambayo wakaaji na hata wasiowakaaji wa Kesses wamepata na wanazidi kujinufaisha kwalo. Hata hivyo,bwawa hilo Lina nuksi zake hapa na kule huenda hazina mashiko sana kwa wanaonufaika. Kwa makala haya tutaangazia jinsi ambavyo bwawa hili lilianzishwa na kwa sababu zipi ama historia yake na kisha manufaa na madhara yake kwa wakaaji iwapo yapo,jina langu ni Lydia Omaya.

Wanafunzi wa chuo kikuu cha Moi wakiendeshwa kwa mashua katika bwawa la Kesses.

Bwawa la Kesses lilianzishwa mwaka wa elfu moja mia tisa arubaini na saba hadi mwaka wa elfu moja mia tisa hamsini na mbili na wazungu waliokuwa wamejinyakulia mashamba maeneo haya ya Kesses. Kusudi kubwa la kuanzisha bwawa hili lilikuwa uogeleaji. Katika shughuli zao za ukulima, wazingu hao walihitaji maji ya kunyunyizia mimea yao ili ipate kunawiri na kutoa mazao mazuri. Mwaka wa elfu moja mia tisa themanini mashua yaliingizwa katika shughuli za kuendeshwa kwenye bwawa hili la kesses. Hii ilikuwa njia moja ya kipekee ya kuwaburudisha wazungu waliokuwemo wakati huo.
Ukubwa wa bwawa hili lilisababisha kuanzishwa kwa chuo kikuu cha Moi ambacho hakipo mbali na bwawa hili. Hii ni kwa sababu maji katika bwawa hili yanatosha katika shughuli za usambazaji sio kwa chuo kikuu cha Moi tu bali kwa wakaaji wote, wa mbali na karibu. Hadi sasa bwawa hili limebaki kuwa la burudani haswa kwa wanafunzi wa chuo cha Moi ambao huzuru bwawa hili mara kwa mara kwa ajili ya kufurahia mandhari mazuri yalioko hapa na zaidi kuendeshwa kwa mashua.
Moja kati  ya mashua zinazotumika katika bwawa la Kesses. 


Maji kutoka bwawa hili pia huelekea
kwenye maporomoko ya maji yalioko ndani ya chuo kikuu cha Moi. Maporomoko haya ya maji pia hufurahisha macho ya wanafunzi wanaotembelea huko. Shughuli za kuogelea pia hufanyika hapa mara kwa mara mbali na shughuli zingine kama vile kufua nguo,kunywesha mifugo na matumizi mengine kwa wanakijiji. Bila maki haya shughuli  nyingi hazingeendelezwa. Kampuni ya Eldowas ilianzishwa kwa ajili ya bwawa hili. Inafukuta maji yaliyotibiwa kwa wanakijiji,  wakaaji wa Kesses na hata chuo kikuu cha Moi ambacho kilijengwa maeneo haya kwa sababu ya kupata maji kwa urahisi kutoka kwa bwawa hili.


Mbali na hayo yote,bwawa hili limewafaidi watu wengi sana na kuwawezesha kujikimu kimaisha. Wakiwemo waendeshaji pikipiki wanaobeba wanafunzi kuelekea bwawa na hata  kurudi,waendeshaji mashua pia wanalipwa kwa shughuli hiyo ambapo mtu mmoja analipa shilingi hamsini. Isitoshe,shughuli za uvuvi huendelea katika bwawa hili . Wavuvi huuza samaki ambacho ni chakula kinachopendwa na wengi haswa wanafunzi wa chuo cha Moi. Vyakula pia huuzwa kwenye bwawa ambapo pia kuna pesa za kiingilio zinalipwa.Kwa njia hii wafanyabiashara hawa wanaweza wakajimudu kimaisha na hata kuwalipia karo watoto wao. Kwa kuendesha mashua,siku za wikendi huwa bora zaidi. Wanafunzi huwa wengi kuliko siku zingine za wiki.



Ni mengi yamesemwa kuhusu bwawa hili la Kesses ambalo bado serikali haijaingilia kati ili kuimarisha usawa wake. Kuna baadhi ya magugu yameenea kwenye bwawa hili na basi kufunika sehemu kubwa ya maji kadri muda unaposonga. Swali labakia kuwa je,serikali itaskia kilio cha wakaaji wa eneo hili la Kesses na kisha kuingilia kati na kuimarisha shughuli katika bwawa hili la Kesses?
Magugu yalivyoenea katika bwawa la Kesses. 


Haya ndio makala yetu ya bwawa la Kesses, jina langu ni Lydia Omaya.

Comments

Post a Comment

Leave a comment

Popular posts from this blog

MOTHERLAND